Mshambuliaji
wa kutegemewa wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi
amesema kuwa imemuuma sana kukosa penati iliyosababisha kutoka sare ya
1-1 na Iceland kwenye mechi ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia.
Mkwaju
wa penati wa Messi ambao ulivuta lenzi za macho ya wengi uliishia
mikononi mwa mlinda mlango Hannes Halldorsson na kuzima matumaini ya
Argentina kujitwalia alama tatu muhimu.
Messi
anatazamwa akisaka kuifikia rekodi ya mshindani wake Cristiano Ronaldo
ambaye alifanikiwa kupata ‘hat-trick’ kwenye mechi nzito kati ya Ureno
na Uhispania, Ijumaa iliyopita.
“Kwa kawaida inauma sana kukosa penati. Kama wangefungua zaidi tungeweza kupata nafasi zaidi,” alisema Messi.
“Tuna
uchungu wa kushindwa kuzipata alama tatu ambazo tulistahili. Kuanza na
ushindi ni muhimu wakati wote, sasa tunatakiwa kuanza kufikiria kuhusu
Croatia. Tutajaribu kulipita hili haraka,” aliongeza.
Alisema
kuwa mbinu ya Iceland ilikuwa ngumu kwa upande wake kwakuwa wahakutaka
kucheza sana bali walijikita katika kuziba lango lao.
Croatia ambayo inasubiri kukutana na Argentina pamoja na Iceland, jana ilijitwalia alama 3 muhimu baada ya kuifunga Nigeria 2-0.
Magoli ya Croatia lilitokana na Oghenekaro Etebo kwa kujifunga (dakika ya 32) na Luca Modri (dakika ya 71) kwa mkwaju wa penati.


0 Comments